WAPIGANAPO FAHARI WAWILI ZIUMIAZO NI NYASI

Christina Mande
Wisdom&Wellness Counselor

Kizinga, Dar-es-Salaam

Katika familia, kama baba na mama wanagombana kila wakati, watoto ndio wanaoteseka kwa kukosa huduma za msingi hasa kama itatokea baba na mama wanatengana/kuachana.

KATIKA MAISHA KUNA KUPATA NA KUPOTEZA

Grace Mshanga
Wisdom&Wellness Supervisor

Temeke & Ubungo,Dar-es-Salaam

Usemi huu huhamasisha kutunza utajiri. Ukipata utajiri uwe mwangalifu sana. Kwa mfano, inawezekana ulikuwa na mabasi ya abiria 10, mwisho ukapoteza kila kitu ukakosa hata baiskeli ya magurudumu mawili.

CHEMA CHAJIUZA, KIBAYA CHAJITEMBEZA

Rustica Tembele
Founder & CEO

Maana yake, kitu kizuri hakiihitaji matangazo, uzuri wake huonekana kwa uwazi, lakini kitu kibaya huhitaji kutangazwa na hutembezwa ili watu wakione.

Msemo huu unaweza kutumika pale mtu anapojigamba sana mbele za watu kuwa yeye ni wa hivi ama vile, lakini watu hawavioni hivyo anavyojigamba navyo bali wanamuona kama mtu wa kawaida tu.

MALI BILA DAFTARI HUPOTEA BILA HABARI

Suzan Mwingira
Administrative Assistant

Msemo huu unamaana kwamba ni vema kuweka kumbukumbu za vitu vyako katika mahali pa usalama na katika mpangilio mzuri au kupangilia kazi zako kwa ufasaha zaidi ili kukuwezesha kujua, kutambua kwa urahisi mwenendo mzuri wa kazi zako au biashara yako.

UKIPENDA BOGA, UPENDE NA MAUA YAKE

Christina Mande
Wisdom&Wellness Counselor

Kizinga, Dar-es-Salaam

Ukimpenda mtu mpende na makandokando yake. Ina maana kuwa unapompenda mtu uwe tayari kupenda mazuri yake pamoja na yale ambayo hayakupendezi. Hali kadhalika, wapende ndugu zake na wa wale wote anaohusiana nao, usibague.

HAKUNA NJIA NDEFU ISIYO NA MWISHO

Grace Mshanga
Wisdom&Wellness Supervisor

Temeke & Ubungo,Dar-es-Salaam

Hii huwafundisha na kuwaweka tayari wanandoa wapya kuwa hata tatizo liwe kubwa na limedumu kwa muda kiasi gani, mwisho wake ni kusamehana na kuishi kwa furaha na amani kama mwanzo.

UNAPOFANYA KAZI NI ADHA TU, MAVUNO YAKIWA TAYARI NI VICHEKO

Grace Mshanga
Wisdom&Wellness Supervisor

Temeke & Ubungo,Dar-es-Salaam

Katika hali ya kawaida binadamu kufanya kazi ni adha lakini mapato yapatikanapo ni kicheko. Hivyo vijana na wana ndoa wapya huhamasishwa kufanya kazi kwa bidii ili kupata mavuno bora na mengi ili kujitunza wenyewe na familia zao.

KIDOLE KIMOJA HAKIVUNJI CHAWA


Paulina Ngwawasya
Wisdom&Wellness Supervisor

Ilala & Kinondoni, Dar-es-Salaam


Mwanadamu peke yako huwezi kufanikisha malengo yako katika maisha kwa kujitenga, unahitaji ushirikiano. Pia ina maana kwamba ushirikiano katika jamii ni muhimu sana kwani ushirikiano huleta maendeleo na mafanikio mazuri katika jamii au kazi. Msemo huu unatukumbusha kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.

%d bloggers like this: