Akufaaye Kwa Dhiki Ndiye Rafiki

Grace Mshanga - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Grace Mshanga (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Maisha tulio nayo duniani tunaishi kwa kuwa na marafiki mbalimbali, katika hao wanawezekana kuwepo wale wa kutaka wewe uwasaidie daima. Watakuwepo pia wale wa kushikamana nawe kwenye raha tu, mfano sherehe mbalimbali, n.k.

Lakini rafiki wa kweli ni yule anayeshikamana nawe wakati ufikwapo na shida mfano umefiwa, umeunguliwa nyumba, umepata ajali nk, huyo ndiye rafiki anayakufaa kwa dhiki.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Heshima ni Msingi wa Maelewano Duniani

Alfreda George - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Kulikuwa na dada mmoja ambaye alikuwa akijiona kuwa maisha ameyashinda na kwamba hana shida yoyote hapa duniani. Kwa vile alijiona kuwa Yeye ni ‘matawi ya juu’hakuna sababu ya kupoteza muda wake kuongea ama kushiriki ana na watu wa hadhi za chini. Alijitenga na kukaa mbali na jamii inayomzunguka, hakutaka kuongea na yeyote. Hata watoto wake hakutaka wakaribiane ama kucheza na watoto wenzao.

Siku moja akiwa kazini mtungi wa gesi ulileta hitilafu, msichana wa kazi alishutuka na kuogopa sana. Badala ya kutoka nje na kukimbia na watoto aliingia nao chumbani na kujifungia. Moto ulianza kuwaka na kusambaa haraka sana. Majirani aliokuwa ana wadharau na kuwaona si lolote mbele yake, walipoona nyumba inaungua na pia waliposikia kelele za watoto wakilia mle ndani, waliikimbilia nyumba, wakabomoa dirisha la chumbani na kuwatoa wale watoto. Watu ambao alikuwa anawadharau ndio waliokuja kumsaidia. Sebule na vyumba vyote vilishika moto. Msichana wa kazi na watoto wa mwenye nyumba walitolewa na majirani wakasalimika adha hiyo ambayo ingepelekea umauti wao. Lakini hakuna kitu hata kimoja kilichotoka mle ndani, vyote viliungua kabisa na moto. Hasara ilikuwa kubwa sana.

Majirani waliokuwa wakidharauliwa na mama huyo ndio waliotoka kumsaidia kwenye hili tukio la moto. Pamoja na kumsaidia kwa moyo moja walisikika wakimsema vibaya sana. Wangekuwa na roho mbaya wasingeweza hata kuwasaidia watoto wake.

Mama mwenye roho mbaya aliporudi toka kazini aliona yaliyotokea na kusikitika sana. Alipata fundisho kubwa sana. Aligundua kuwa wale aliowaona ni wajinga ndio waliowaokoa watoto wake.

Hadithi hii inatufundisha kutowadharau watu, inatupasa kumheshimu kila mtu bila kuangalia hali zao. Tuache kuwadharau watu hata kama hali zao ni mbaya kiasi gani kwani watakusaidia wakati wa matatizo. Na siyo hivyo tu, kila
binadamu ana haki ya kupendwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa. Kwa maana hiyo, inatulazimu tuwe na mahusiano mazuri na binadamu wenzetu kwani mwanadamu siyo kisiwa, anaishi na watu. Heshima ni kitu cha bure lakini kina thamani sana. Ni lazima tutunze na kuomyesha kwa kila awaye katika maisha yetu ya kila siku hapa duniani.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Mstahimilivu Hula Mbivu

Tap Elderly Women's Wisdom for Youth (TEWWY)

Masimulizi …

by Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY).

Binadamu wengi mara nyingi tunapohitaji ama kupanga mambo huwa tunapenda yatokee mapema iwezekanavyo. Wala siyo ajabu kuwa na mategemeo hayo, ni ubinadamu, ni kawaida kabisa.

Kila mtu ana haki ya kuwa na ndoto, ndoto za jinsi maisha yake yawe. Wakati mwingine huwa ni ndoto za Alinacha, ndoto za kusadikika. Kuna hadithi ya kijana mmoja jina lake Rahim aliyebahatika kusoma hadi kufika Chuo Kikuu. Ndoto ya kusoma alikuwa nayo tokea akiwa mdogo na Mungu kwa hakika alimbariki hadi akatimiza ndoto yake.

Baada ya kumaliza na kupata digrii yake matarajio yake yakapanuka zaidi. Alijiona kuwa sasa ana nafasi na haki ya kupata kazi kubwa ya kufanana na hadhi yake kwani kisomo chake kilikuwa ni kikubwa. Mungu alimjalia akapata kazi ya kawaida tu na siyo kubwa vile alivyokuwa anatarajia . Aliifanya kazi hiyo kwa bidii zake zote kwa muda wa miaka saba hivi na kwa mshahara ule ule alioanzia. Wenzake waliokuwa nyuma yake walipata kazi nzuri zaidi zenye mishahara mikubwa. Walimshawishi aache kazi pale na atafute sehemu nyingine yenye mshahara mkubwa zaidi.

Rahim alitafakari ushauri huo ambao kwa upande ulikuwa ni mzuri, pengine kimaslahi zaidi. Mawazo yalimjia kichwani, kwa upande moja alivutiwa kusikiliza ushauri wa wenzie na upande mwingine roho ikawa inasita. Baada ya kuishauri nafsi yake kwa dhati aliamua kuituliza roho yake pale alipo. Alimuomba Mwenyezi Mungu amsaidie kufikia maamuzi sahihi. Aliona ni vema kuwa na subira ili avute kheri.

Aliendelea kusubiri, na alisubiri sana kwani ilipita miaka mingime kumi kabla historia yake mpya haijaanza kuandikwa.

Siku moja akiwa kazini kwake alipigiwa simu na Mkurugenzi Mkuu (MK) wa shirika moja la kimaifa hapa nchini. Mazungumzo yalikuwa hivi: “Naongea na ndugu Rahim”?, sauti
nzito na yenye madaraka ilisikika kutoka upande wa pili. “Naam, ni mimi”, sauti iliyosheheni adabu ilijibu. Mkurugenzi alendelea: “mimi ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Kimataifa. Ninakuhitaji uje siku ya Alhamisi ofisini kwangu saa 4 asubuhi.” Alimuelekeza ofisi hiyo ilipo ili asipate tabu kuitafuta.

Alhamsi ilipofika saa tatu na nusu alikuwa tayari pale ofisini akisubiri. Ilipofika saa 4 kamili mhudumu wa ofisi alienda kumwita Rahim aliyekuwa ametulizana pale mapokezi akisubiri. Alisimama na kufuatana na yule mhudumu hadi mlangoni kwa MK. Alipoingia alikaribishwa kwa furaha, MK alianza kwa kusema: “Nimefurahi sana kukuona na ninakushukuru kuitikia wito wangu”. Aliendelea, “nimekuita kwa sababu ninamtafuta mtu anayefaa kushika nafasi ya MK katika shirika hili. Nimekuwa nawafuatilia watu wengi ili kuweza kupata mtu anayefaa. Mimi karibu naondoka kurudi Ulaya na hivyo ningependa kumpata mzalendo aweze kushika nafasi hii. Watu zaidi ya kumi wamechunguzwa kwa ajili ya nafasi hii. Baada ya kushauriana na watu wengi kutoka Serikali ya Tanzania imeonekana kuwa wewe, Rahim ndiye kijana unayefaa kushika nafasi hii. Ningependa kujua unasemaje kuhusu fursa hii. Siyo lazima unijibu leo, bali nakupa muda wa siku tatu kufikiri ili baada ya hapo uweze kunipatia majibu”, MK alimaliza.

Rahma alipigwa na butwaa asiweze kujibu lolote zaidi ya kububujikwa na machozi. Hakuwahi kutegemea kabisa kusikia na kupata muujiza kama huo katika maisha yake. Hatimaye, Rahim alipata nguvu ya kwenda kumshukuru MK kwa nafasi hiyo. Baada ya siku tatu alirudi kwa MK na kuikubali nafasi hiyo ya pekee.

Tunajifunza nini kutoka simulizi hii? Yapo mengi ya kujifunza lakini yafuatayo ni ya msingi zaidi:

 1. Kutumikia nafasi tunazozipata kwa umakini na kwa bidii. Umakini katika kazi ndio uliomfikisha Rahim hapo.
 2. Kutulia mahali pamoja kwenye sehemu ya kazi kunakujengea historia fulani na inakuwa rahisi kufuatilia historia yako. Rahim alitumikia kwenye ajira aliyokuwa nayo kwa zaidi ya miaka 16. Kama angekuwa anaacha acha ajira, mara hapa, mara kule isingekuwa rahisi kufuatilia sifa zake za kiajira. Uvumilivu wake ulimwezesha Rahim kutengeneza historia ya utendaji wake wa kazi. Kampuni hiyo ya kimataifa iliweza kupata utendaji wa kazi wa Rahim kwa urahisi sana kupitia ‘referee’ wake.
 3. Tunajifunza bayana kuwa ‘Subira huvuta kheri / Mvumilivu hula mbivu. Miaka mingi aliyofanya kazi kwenye
  ajira yake haikumfannya azorote kwenye utendaji wake. Alifanya kazi kwa bidii, akaonekana kutokana na utulivu wake wa kukaa sehemu moja ya ajira muda mrefu. Hatimaye alionekana, akainuliwa.

Swali la kujiuliza: wewe unayesoma simulizi hii, una uvumilivu kiasi gani? Jifunze kutoka hadithi hii, subira na uvumilivu wako vitakulipa, ipo siku utainuliwa!

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Asiyefunzwa na Mamaye, Hufunzwa na Ulimwengu

Tap Elderly Women's Wisdom for Youth (TEWWY)

Masimulizi …

by Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY).

Ni jukumu la wazazi kuwapa malezi mazuri na mema watoto wao. Mwalimu wa kwanza wa mtoto ni wazazi. Malezi haya yanatakiwa yaanze tokea siku ya kwanza mtoto anazaliwa. Ikumbukwe kuwa mtoto anapozaliwa anakuwa kama karatasi nyeupe kabisa isiyo na doa ama alama yoyote. Mzazi/mwezi anakuwa wa kwanza kabisa kuandika katka karatasi ile nyeupe. Akianza kwa kuandika mambo yasiyofaa yatabaki kwenye karatasi ile. Hali kadhalika akiandika mambo mazuri pia yatabakia kwenye hiyo karatasi. Huo ndio mwanzo wa kumjenga mtoto, vizuri ama vibaya. Kwa maana nyingine, utakavyomlea mtoto wako ndivyo atakavyokuwa, mathalan kuwa na adabu njema kwa watu ama kutokuwa na adabu, kuwa jeuri kwa watu ama kuwa mtii, kuwa na nidhamu ama kuwa mtovu wa nidhamu

Ni rahisi sana kwa watu wamuonapo mtoto kwa mara ya kwanza kujua malezi aliyopata. Matendo na maneno ya mtoto aliyelelewa vizuri ni tofauti sana na ya yule aliyelelewa vibaya. Mathalani, kama mtoto ameanza kuonyesha tabia mbaya kama ya utovu wa nidhamu na wazazi wakamwacha tu aendelee kukosa adabu, huko hakutakuwa ni kumpenda; ni kumdhuru. Kwani mtoto huyo akija kuwakosea watu wengine, hawatamuachia. Watampiga, na pengine vibaya zaidi kuliko ambavyo wangalimpiga wao wenyewe pale alipokuwa mdogo. Mara nyingi mafunzo ya ulimwengu ni ya kikatili, hayana huruma hata kidogo.

Kuna mipaka katika kuwapenda watoto wetu. Tusiwaharibu kwa kisingizio cha kuwapenda kwani tukifanya hivyo tutakuja kujuta pale ulimwengu unapochukua nafasi yetu ya kuwafunza kama wazazi. Na ikifikia hatua mtoto akaambiwa maneno haya ya asiyefunzwa na mama hufunzwa na ulimwengu, na bahati mbaya endapo wazazi
wakayasikia, wanaweza kuumia sana kwani pamoja na kwamba yanaelekezwa kwa mtoto, mzazi pia analaumiwa. Haiwi lawama kwa mtoto tu bali na kwa wazazi pia ambao mnaonekana dhahiri mlishindwa kutimiza wajibu wenu kama wazazi.

Somo hili ni zuri kwa watoto na kwa wazazi pia, hali kadhalika, na kwa wale ambao hukataa kusikiliza maoni au ushauri wa wengine kwani mwisho wa siku huangukia kwenye mikono ya walimwengu.

Hima wazazi tutimize wajibu wetu kama wazazi; hali kadhalika watoto mzingatie malezi ya wazazi ili msije mkaingia kwenye darasa la walimwengu.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Umakini Katika Kufanya Maamuzi ni Muhimu

Margaret Kayombo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Hapo zamani za kale, baada ya kuumbwa ulimwengu na vitu vyote ndani yake pamoja na watu. Mungu alifikiria sana juu ya uhai wa wanadamu. Alifikiri endapo itakuwa sahihi iwapo wanadamu wataishi milele bila kufa kama yeye Muumba au wafe baada ya kuishi ulimwenguni kwa muda fulani. Baada ya fikra hizo, hatimaye aliwatuma viumbe wawili wakawaambie wanadamu kuwa yawapasa wafanye maamuzi wenyewe kuhusu fikra zake hizo.

Kwanza alimtuma kinyonga na kumpa ujumbe huu. Kinyonga aliupokea ujumbe na kuelekea ardhini. Aliwaambia binadamu kama alivyoagizwa na Mungu kwa kusema: “Mmeambiwa msizaane, mbaki nyie wawili tu ulimwenguni, mke na mume na msife ila muishi milele”

Kisha Mungu akamtuma njiwa na ujumbe ambao ulikuwa tofauti na ule aliopewa kinyonga. Njiwa alianza kwa kuwaambia wanadamu: “Mungu ameniagiza niwaambie kuwa mkitaka mzaane kisha mfe. Mkifa uhai utaendelezwa na watoto, wajukuu, vitukuu, vilembwe, vilembekeza na vinying’inya vyenu”. Njiwa aliendelea kusema, “Kwa jinsi hiyo, ijapokuwa nyinyi wenyewe mtakufa, dunia haitakuwa tupu bali itaendelezwa na hao mtakaowazaa na watakaowazaa na watakaozaliwa. Nanyi mtakumbukwa milele.”

Pamoja na kwamba kinyonga alikuwa wa kwanza kutumwa na Mungu, kwasababu ya mwendo wake wa pole pole, mbele na nyuma, alifika muda moja na Njiwa. Kinyonga alipofika alianza kutoa ujumbe wake na watu walimkemea na kumcheka kwa kuwacheleweshea ujumbe wao. Hawakuwa na subira hivyo hawakumtaka kinyonga azungumze. Walimruhusu njiwa atoe ujumbe uliotoka kwa Mungu kabla ya Kinyonga hajafanikiwa kufanya hivyo. Chapuchapu Njiwa alitoa ujumbe wake kama alivyoagizwa. Alifanikisha kuuwasilisha japo ulikuwa mrefu lakini ujumbe uliwafikia. Wakausikiliza kwa makini, wakauona ni ujumbe mzuri, wakaukubali. Walipokubali tu, Kinyonga naye akakubaliwa kuuhitimisha ujumbe wake aliokuwa ameanza kuutoa na akasitishwa asiendelee. Baada ya binadamu kuusikiliza ujumbe wa kinyonga waliuona kuwa ni mzuri kuliko ule wa njiwa kwani kama wangeuchagua wasingekuwa wanakufa, wangeishi milele. Walitaka kuubadilisha uamuzi wao kwani ni dhahiri kuwa watu hawapendi kufa.

Hapo sauti ya Mungu ikasikika ikisema kwamba kubadilisha haiwezekani, sababu alikuwa amekwishapokea tayari uamuzi wao na tayari ameukubalia. Binadamu walipotaka kumuuliza maswali maswali sauti hiyo ilitoweka ghafla hivyo hawakuweza kufanya chochote. Muda ulikuwa umekwisha. Hivyo basi kuanzia hapo wanadamu wakaanza kuzaana na kufa.

Kuna mengi ya kujifunza hapa.

 1. Tuwe waaminifu na kutimiza wajibu wetu kwa wakati.
 2. Tufikirie kwa makini kabla ya kufanya maamuzi
 3. Tusiwe vigeugeu wakati wa kutoa maamuzi yaliyo sahihi.
 4. Tuishi na kujua daima kwamba yupo mwenye maamuzi ya mwisho juu ya kila kitu.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Je, Rafiki Ni Nani Katika Maisha Yako?

Margaret Kayombo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Siku moja mjomba alitufafanulia aina ya marafiki. Alisema kuna rafiki mzuri na rafiki mbaya.

Binadamu ni kiumbe ambaye huhitaji kuwa na rafiki ili aweze kuondoa ukiwa na pia kupata faraja. Kwa kawaida marafiki hufahamiana, huzoeana na huchangamkiana katika maongezi yao mbalimbali. Marafiki huweza kupatikana popote, yaani katika mazingira ya nyumbani, shuleni, kazini, msikitini, kanisani na hata safarini. Ni dhahiri kwamba ushauri wa marafiki huwa una nguvu na rahisi kuweza
kuambukizana tabia.

Rafiki anaweza kusababisha huzuni badala ya kuleta furaha. Kwa hiyo, ni muhimu kuchunguza kwanza tabia ya mtu unayetaka kuanzisha naye uhusiano. Ni heri kukosa rafiki kuliko kuwa na rafiki mlevi, mwongo, mwizi, mvivu, mwenye dharau au mwenye tabia nyingine mbaya. Rafiki wa kufaa ni yule mwenye adabu, busara na mwaminifu. Vile vile ni yule anayekutakia mafanikio mema katika maisha yako badala ya kukusababishia matatizo. Kwenye mazungumzo haya ya busara nimepata masomo yafuatayo:

 1. Umuhimu wa wazazi kuwa makini sana na watoto juu ya marafiki wanaokuwa nao kwenye mahusiano.
 2. Kuna marafiki wa kweli na marafiki wa uwongo. Inatupasa kuwachunguza sana, na ukigundua siyo marafiki sahihi inatubidi kuachana nao mapema na inabid Uwe tayari kwa lolote linaloweza kutokea.
 3. Kuna marafiki wengine wanataka kuwatumia ama kuwapeleka pabaya wenzao ili waangamie kama wao walivyoangamia kwa hiyo ni vema kuwa waangalifu na aina ya marafiki wa hivyo.
 4. Kuna marafiki wengine ni vigeugeu kwa hiyo hao nao pia yakupasa uchukue muda kuwajua vizuri kabla ya kuanza mahusiano nao.

Watu wengi, hususan vijana huishia pabaya kutokana uchaguzi mbaya wa marafiki . Yatupasa kuchukua tahadhari

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Atafutaye Hachoki, Akichoka Keshapata

Margaret Kayombo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Kwa kawaida, mtu anayekitafuta kitu huwa hachoki, huendelea kutafuta mpaka akipate. Endapo ataonyesha dalili za kuchoka basi watu husema kuwa amekwishapata kile alichokuwa akikitafuta.

Mtu mwenye bidii katika jambo hufanikiwa katika lengo lake. Kwa usemi huu tunahimizwa kuwa na juhudi au bidii katika kazi au jambo lolote tunaloshughulika nalo kama tunataka kufanikiwa. Hata kama tusipoyaona matunda ya bidii au juhudi zetu kwa muda huo tusikate tamaa kwani ipo siku tutafanikiwa tu. Mambo magumu tunayoweza kuyapitia ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Yatupasa kuwa na uvumilivu usio na kikomo ili hatimaye tuweze kufanikiwa katika maisha yetu.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Uhusiano wa Nidhamu Binafsi na Uchumi Katika Maisha

Caroline Swai - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Alikuwepo msichana mmoja ambaye alizaliwa katika kijiji kimoja na alilelewa kwa malezi bora na akawa na nidhamu ya hali ya juu. Wazazi wake walijitahidi kwa uwezo wao wote wakamsomesha hadi darasa la tatu tu.

Binti huyo alikuwa na nidhamu binafsi kwani alikuwa mtiifu kwa kila mtu pia alikuwa na nidhamu, akisalimia anapiga magoti, anapokuwa anampatia mtu kitu napo pia anapiga magoti. Kwa ujumla alikuwa na tabia nzuri mno.

Baada ya kushindwa kuendelea na shule ya msingi kutokana na hali duni ya kiuchumi ya wazazi alienda kufanya kazi za ndani kwa familia moja ya wasomi. Baba wa familia hiyo alikuwa Profesa, watoto wake kila mmoja alikuwa na digrii mbili kutoka Vyuo Vikuu vya nje vinavyoeleweka. Ni dhahiri kwamba hii ilikuwa ni familia ya wasomi watupu.

Profesa huyo alikuwa anafundisha Chuo kimoja maarufu hapa nchini. Kama ilivyo kawaida kwa maprofesa wa Vyuo vikuu, alikuwa na jukumu la kumsimamia mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu ambaye alikuwa anachukua digrii yake ya tatu. Hivyo kijana alikuwa anamfuata Profesa nyumbani kwake kwa ajili ya kusahihishiwa kazi zake mara kwa mara.
Profesa alikuwa akiacha maagizo kwa dada wa kazi kuwa kama kijana huyo akija amkaribishe na amhudumie kwa kumpa kinywaji anachotaka na awe anaangalia mara kwa mara ili kama amemaliza kinywaji amwoongezee. Dada wa kazi alipokea maagizo kutoka kwa bosi wake na aliyafuata barabara.

Mwanafunzi huyo alipokuja kwa mara ya kwanza nyumbani kwa Profesa dada wa kazi alimpokea kwa uchangamfu, akamsalimia kwa kupiga magoti na akamuhudumia kama alivyoagizwa, huku akipiga magoti pia. Isitoshe alikuwa anaenda kumuangalia mara kwa mara ili aweze kumhudumia zaidi.

Wakati huo huo wale mabinti wa Profesa, wakiwa na simu zao za hali ya juu na vimini vyao vya nguvu wakipita wanamsalimia yule kijana kidigitali “Hi”. Walikuwa hawapigi magoti kwani hawajazoea kufanya hivyo na baada ya hapo waliishia zao na kuendelea kuchati na kucheza game kwenye laptop zao.

Kijana yule mwanafunzi akawa anaona tofauti kubwa sana kati ya dada wa kazi na mabinti wa Profesa. Alivutiwa sana na nidhamu binafsi ya dada wa kazi.

Baada ya kumwangalia binti wa kazi kwa muda mrefu yule kijana ilibidi amweleze ukweli kuwa amevutiwa naye na angependa kumuoa. Dada alishtuka sana na kumweleza kuwa haiwezekani kwa sababu yeye amesoma hadi darasa la tatu tu na hajui mambo mengi. Badala yake alimshauri amweleze mmoja kati ya dada zake, yaani watoto wa Profesa kwa sababu wao ndio waliosoma sana kama yeye. Kijana akamjibu kuwa, amewaona hao mabinti lakini amoona kuwa hawasomeki, tabia zao siyo nzuri, hawajitambui, mavazi yao siyo ya heshima, hawajui kusalimia kwa nidhamu. Kwa ujumla, alimalizia kuwa hawana nidhamu. Bila kumung’unya maneno alisema kuwa hayupo hata mmoja kati yao anayefaa kuwa mke.

Yule kijana aliendelea kumshawishi dada wa kazi hadi akakubali kuolewa naye. Kijana alimweleza Profesa kuwa anataka kuchumbia kwenye familia yake. Aliomba kibali cha kuleta barua ya kuomba uchumba.
Profesa kusikia hayo alifurahi sana kwani alitarajia kuwa barua hiyo itakuwa inamhusu mmoja wa binti zake kwani kamwe asingefikiria kuwa msichana wa kazi ameuteka moyo wa kijana. Kwa furaha kubwa, Profesa alimkaribisha kijana nyumbani kwake kuleta barua hiyo.

Kijana alijiandaa barabara, akawa tayari kuileta barua ya kuposa kwa Profesa. Barua ilipokelewa kwa furaha sana lakini Profesa alipoifungua alikutana na jina la dada wa kazi badala ya jina la mmoja wa binti zake. Profesa alichanganyikiwa, hakuelewa maana ya kile anachokiona mbele yake. Alivua miwani yake, alidhani pengine hakuisoma vizuri barua hiyo. Akarudia kuisoma mara mbili zaidi. Lakini haikusaidia kwani haikuwa hivyo alivyokuwa anategemea. Binti wa kazi ndio alikuwa anaposwa kweli, haikuwa utani.

Kutokana na mkanganyiko huo, ilimlazimu Profesa kuahirisha hafla hiyo ya upokeaji wa barua. Kesho yake Profesa alimwita kijana akamwuliza: “mbona barua uliyoleta sikuielewa? Mbona ilikuwa na majina ambayo hayaeleweki na siyo ya mmoja wa binti zangu? Umechanganyikiwa, ama? Naona itabidi nikufanyie unasihi sasa mimi mwenyewe”.

Kijana alimsikiliza kwa umakini Profesa wake kisha akamwambia: “mimi sijachanganyikiwa hata kidogo, akili zangu ziko timamu kabisa. Ninayetaka kumposa ni huyo huyo niliyemuandika jina lake. Ninamaanisha huyo dada wa kazi za ndani hapo nyumbani kwako. Isitoshe Profesa, suala la mke ni moyo unaoamua na si vingine.

Baada ya kusikia hayo, Profesa hakuwa na la kusema tena. Ilibidi aache kuliongelea jambo hilo. Alimwambia kijana kuwa, itabidi wazazi wa dada wa kazi waitwe ili waje kupokea barua ya binti yao, kwani huo ndio utaratibu wa mila zetu.

Wazee waliitwa na kuja. Waliipokea barua hiyo na hatimaye ndoa ikafungwa.

Baada ya ndoa, bibi harusi alimweleza mume wake kuwa ana hamu ya kusoma. Mme wake alimruhusu akaanza kusoma na akawa anamsaidia pia pale nyumbani. Hatimaye aliweza kufika Chuo Kikuu na leo hii ana digrii tatu kama mume wake na wanaishi Marekani.

Kwa upande wa watoto wa Profesa hali zao ziliendelea kuwa ni zile zile za kutokuwa na nidhamu binafsi, kutojitambua, na kutokutumia vizuri fursa walizokuwa nazo. Wasichana hawa waliishi maisha yasiyokuwa na mwelekeo, walishindwa kuwatunza hata watoto wao waliowazaa wenyewe mpaka ikafikia yule aliyekuwa dada wa kazi akaamua kuubeba mzigo wa kuwatunza watoto wao.

Majukumu yale ya dada wa kazi hayakuishia hapo tu kwani alijikuta akiwatunza hata waajiri wake wa zamani, yaani Profesa na mkewe kwani walikuwa wamekwishazeeka na wakawa hawapati msaada wowote kutoka kwa watoto wao. Wazee hawa walikuwa wakipata huduma zote pamoja na huduma za afya kutoka kwa dada huyo.

Kutokana na hadithi hii ambayo ni ya kweli, tunafundishwa kuwa nidhamu kwani ni msingi wa maendeleo yetu. Huyu msichana wa kazi katika hadithi hii alifika hapo alipofikia kutokana na nidhamu yake. Lakini nidhamu hii siyo kwenye kupata wachumba tu bali ni kwa kila kitu ambacho tunakitenda hapa duniani. Nidhamu huzaa vitu vingi kama upendo, amani, furaha na heshima. ‘NIDHAMU BINAFSI NI MSINGI WA MAISHA NA MAENDELEO KATIKA KILA NYANJA ZOTE.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Majivuno na Kiburi ni Adui wa Maendeleo

Margaret Kayombo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Katika maisha ya mwanadamu hapa duniani majivuno na kiburi ni kikwazo cha kukurudisha nyuma kimaendeleo.

Katika nchi moja kulikuwa na mfalme mmoja mwenye maringo na dharau sana, aliwaona watu wake kama sio binadamu. Raia wake walikuwa wanamchukia sana, hata wakamwombea afe. Siku moja alipokuwa anahutubia kwenye mkutano wa wazee alithubutu kusema kuwa yeye hajawahi kuiona njaa na angefurahi sana kama angempata mtu ambaye angeweza kumuonyesha njaa ilipo na inafananaje, kwani huwa anasikia tu kuwa duniani kuna njaa.

Wazee walikasirishwa sana na kauli zake hizo za mara kwa mara. Ndipo mzee mmoja mwenye busara akajitolea na kwenda kumweleza mfalme ya kuwa, yeye yupo tayari kumpeleka na kumwonyesha njaa ilipo, Mfalme alikubali kwenda na huyo mzee ili akaione njaa kwa macho yake.

Mzee yule alitengeneza mikate yake saba na akamwambia mfalme kuwa safari imejiri. Pia alimwambia mfalme asichukue kitu chochote, kwani yeye angechukua kila kitu cha lazima pamoja na chakula kwa ajili ya safari yao. Hali kadhalika, alimwambia kuwa hawatatumia chombo chochote cha usafiri, itawabidi waende kwa miguu, maana huko kwenye njaa hakuendeki na gari, njia pekee ni ya miguu tu.

Siku ya kuondoka ilipowadia, walianza safari alfajiri na mapema. Wakaenda mbali sana na kwa vile mfalme hakuzoea kutembea, ilipofika saa sita akawa amechoka ile mbaya. Njaa nayo ikawa inamuuma sana. Yule mzee akafungua mikate yake na kuanza kula peke yake. Kwa vile njaa haina adabu, Mfalme alimuomba kipande cha mkate lakini yule mzee alimnyima. Kwa kebei alimwambia kuwa yule ambaye anasafiri kwenda kuiona njaa huwa hali chochote. Mfalme alivumilia na baada ya kupumzika waliendelea na safari. Ilipofika jioni, maskini mfalme akashindwa kuendelea na safari na kuomba chakula kwa yule mzee.

Baada ya kumuona mfalme yuko hoi bin taaban, yule mzee kwa taratibu alimjibu swali lake mfalme la wapi njaa ilipo. Alimwambia: “hakuna mahali maalumu ambapo ni maskani ya njaa, bali ile anayoihisi ndiyo njaa yenyewe”. Aliendelea kwa kusema: “njaa inamfanya mtu yeyote asiwe na nguvu”. Hivyo yule mzee alimsihi mfalme aweke ahadi kama hatarudia tena vitendo vyake vya majivuno na dharau kwa watu. Asipofanya hivyo kwa kuweka nadhiri yule mzee
atamwacha palepale ili afe kwa njaa. Kutokana na alivyokuwa anajisikia mfalme, wosia wa mzee huyu ulimfanya atii na kuufuata. Mfalme aliapa kwa Mungu kuwa hatarudia tena kuringa, kudharau na kukufuru kama alivyokuwa amezoea.

Hapa tunajifunza mengi nayo ni:

 1. Kama umejaliwa kuwa na utajiri, yakupasa umshukuru Mungu, usiwadharau wale ambao hawana.
 2. Usitumie madaraka uliyopewa kwa ajili ya kuwanyanyasa wengine.
 3. Tuwe na unyenyekevu kwa kila mtu ili siku tutakapopata matatizo wawepo wa kutusaidia..

Hadithi hii inafanana na msemo huu: ‘Adui yako muombee njaa’.
Hapa tumeona pamoja na madaraka aliyokuwa nayo mfalme njaa ilimfundisha kuwa na adabu na utu na hatimaye kuacha majivuno.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Mtoto Umleavyo Ndivyo Akuavyo

Margaret Kayombo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi …

by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).
Fundisho kwa watoto na vijana: “Muwe watii na heshima kwa wazazi wenu”

Palikuwa na mtoto mmoja aliyekuwa anaitwa Ipyana ambaye alikuwa mtukutu na mwenye ghadhabu. Siku moja alimwomba baba yake pesa ili aende kutalii nchi mbalimbali ulimwenguni kwa gharama kubwa. Baba yake alimsihi sana mwanawe asiondoke, lakini Ipyana hakusikia na aliamua kuondoka. Alizunguka huku na huko akiangalia maghorofa, pwani na wanyama kama vile Twiga na huku akitumia pesa ovyo. Miaka ilizidi kwenda lakini Ipyana hakukumbuka kurudi nyumbani, alifurahia mambo mengi mapya na ya kustaajabisha.

Wazazi wake waliona bora wamtafute mtoto wao huenda huko alikoenda alipatwa na masaibu mazito. Walikwenda kila kona lakini hawakufanikiwa kumpata. Kazi nzito na ngumu ilikuwa mbele yao. Kila walikofika, waliambiwa alikuwa hapa lakini alikwishaondoka kwenda nchi nyingine. Wazazi wake walikata tamaa na kusononeka sana. Hatimaye waliamua kurudi nyumbani.

Ipyana alikuwa amewatwisha mzigo mzito mioyoni mwao, mzigo wasioweza kujitua. Waliumia na kukerwa sana na suluba inayosabishwa na mtoto wao. Kutokana na matumizi yake mabaya ya pesa, aliishiwa. Maisha yalibadilika, yakaanza kuwa ya shida. Alianza kukonda kwa sababu ya kukosa lishe. Nguo zake zilianza kumpwaya kabisa. Alihangaika huku na huko kutafuta chakula bila mafanikio. Kwa kuwa alikuwa mtoto mtukutu, watu hawakumsaidia kabisa, akabaki mpweke. Hatimaye alifanya maamuzi ya busara ya kurudi nyumbani kwa wazazi wake ili kuomba msamaha.

Kwa mzazi mtoto ni mtoto, msamaha huwepo daima. Ni sawa na usemi tuliozoea kuusikia: “mkono wako ukishika uchafu huwezi kuukata”, ndivyo ilivyokuwa kwa kijana Ipyana, wazazi wake hawakumtupa, walimsamehe.

Tangu siku hiyo Ipyana alibadili mwenendo wake na kuwa mtoto mwema katika kila jambo.

Hadithi hii ina masomo mawili kwa wazazi, moja, tuchunguze tabia za watoto wetu kuanzia mapema kabisa, na tuwakemee watoto wanapoanza kubadilika. Pili, wazazi tusiridhie kila aombacho mtoto, ni lazima kupima kwanza na kuangalia manufaa ya hicho anachoombea fedha mtoto wako. Pengine Ipyana asingepewa fedha na wazazi wake asingeweza kuondoka na kukutwa na masahibu aliyoyapata.

Kazi kwetu wazazi, tusidekeze watoto bila sababu. Tusiwalee watoto wetu kihasara hasara. Tusichangie kuwaharibu watoto wetu kwa kisingizio cha kuwapenda.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

%d bloggers like this: