HABA NA HABA HUJAZA KIBABA

Sakina Bushiri
Wisdom&Wellness Counselor

Pugu, Dar-es-Salaam

Hii hutumika kuwahimiza watu kuweka akiba, kwani kwa kuweka kidogo kodogo hatimaye utakuwa na akiba ya kutosha 

Msemo huu hutumika kuwaasa watu ambao wana tabia ya kutumia kila wapatacho bila kuweka akiba angalau kidogo. Watu wa namna hii hupata matatizo huko mbeleni kwa kukosa hata mahitaji ya msingi.

NIAMBIE RAFIKI ZAKO NI NANI, NAMI NITAKUAMBIA WEWE NI NANI

Rustica Tembele
Founder & CEO

Maana yake, watu wakijua marafiki unaofuatana nao wanaweza wakajua wewe ni mtu wa aina gani kutokana na tabia za wale rafiki zako, mathalani, kama wana tabia mbaya basi na wewe hautakuwa tofauti nao, vile vile wakiwa na tabia nzuri basi na wewe utafanana nao.

Msemo huu unaweza kutumika pale mtu anapokuwa na tabia zisizotabirika, anapenda kuigaiga na kufanya vitu visivyo vya kawaida. Kwa vile unashindwa kumjua vizuri basi unaweza kumwambia akuambie marafiki zake ni nani ili ujue ni kundi gani unaweza kumuweka.

SAMAKI MKUNJE ANGALI MBICHI

Suzan Mwingira
Administrative Assistant

Msemo huu unatufundisha wazazi na walezi kuwalea na kuwafundisha watoto katika maadili na mienendo mizuri ya  tabia. Hii huwasaidia wanapokuwa katika mazingira yanayowazunguka waweze kukubalika.

Mtoto anapofundishwa angali bado mdogo inamsaidia kujua jambo zuri na baya kadri anavyoendelea kukua katika maisha yake. Hivyo itamsaidia pindi atakapokuwa mkubwa kukubalika katika jamii na hasa katika maswala mbalimbali ya utendaji kazi. Hivyo wazazi na walezi tujitahidi kuwalea watoto wetu katika misingi iliyo imara. Kwa mfano, adabu, heshima nidhamu, umoja, ukweli, upendo na misingi ya kidini.

CHEMA CHAJIUZA, KIBAYA CHAJITEMBEZA

Rustica Tembele
Founder & CEO

Maana yake, kitu kizuri hakiihitaji matangazo, uzuri wake huonekana kwa uwazi, lakini kitu kibaya huhitaji kutangazwa na hutembezwa ili watu wakione.

Msemo huu unaweza kutumika pale mtu anapojigamba sana mbele za watu kuwa yeye ni wa hivi ama vile, lakini watu hawavioni hivyo anavyojigamba navyo bali wanamuona kama mtu wa kawaida tu.