UKISIKIA YOWE KIMBIA KUOKOA JAHAZI

Grace Mshanga
Wisdom&Wellness Supervisor

Temeke & Ubungo, Dar-es-Salaam

Usikiapo yowe lazima kwenda kutatua tatizo. Kuna  sauti maalumu hupigwa ikiashiria tatizo limetokea katika jamii au sehemu hiyo, ni lazima kwenda na kumaliza tatizo kwa ushirikiano.

NDEGE MOJA MKONONI NI WA THAMANI KULIKO KUMI WALIO PORINI

Rustica Tembele
Founder & CEO

Maana yake ni kidogo chochote ulicho nacho ni cha thamani kuliko vingi ambavyo haviko mikononi mwako. 

Msemo huu unaweza kutumika kwa kuwaasa watu wenye tabia ya kudharau kidogo walichonacho na kushabikia/kutamani kikubwa wasichokuwa nacho.. 

MTAKA NYINGI NASAHA, HUMKUTA MINGI MISIBA

Sakina Bushiri
Wisdom&Wellness Counselor

Mangaya, Dar-es-Salaam

Hii hutumika kuwaasa wale wanaopenda kufanya urafiki na kila mtu au kuwafanya kama ndugu zao hukutwa na misiba mingi kwani kila tatizo la mmoja wao litamhusu yeye pia.

Msemo huu unaweza kutumika kwa watu ambao wanapenda kujionyesha ni maarufu na hivyo kutaka waonekane wanashiriki kila jambo litokealo, ukweli ni kwamba siyo rahisi kuwepo kila mahali.

NDEGE MJANJA HUNASA KWENYE TUNDU BOVU

Rustica Tembele
Founder & CEO

Inaweza kuwa na maana ya mtu kufikishwa pabaya pale anapofanya uchaguzi uliopitiliza wa kitu chochote na hatimaye kupata kitu kisicho kizuri. Mathalani, mwanaume anayechagua sana mke au mwanamke anayechagua sana mume anaweza kuishia kupata mke/mume asiyefaa.

Usemi huu unaweza kutumika kwa kuwaasa watu wanaofanya chaguzi zilizopita kiasi kwenye maisha.