Jinsi Ya Kushinda Vita Ya Maneno

Victoria Nakajumo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Victoria Nakajumo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Si kila jambo linalohusu maisha yako lazima umwambie kila mtu. Kadri unavyowaeleza watu mambo yako, ndivyo adui atakavyowafanya wabaya wako wainuke kinyume nawe. Baadhi ya wale utakaowaeleza wataweza kutumia habari zako kukuchafua tu, na si vinginevyo.

Ushauri kwako ni kuwa usiwaamini sana watu, hata wale unaowaita rafiki zako. Usimwamini kila mtu kiasi cha kumweleza mambo yako ya ndani. Ilinde milango ya midomo ya kinywa chako kwa sababu wengine ukiwaamini, hutumia hicho ulichowaeleza kukuharibia maono yako, ikiwa ni pamoja na kukuaibisha. Kumbuka, adui za mtu ni watu wa karibu yake mwenyewe. Kwa hiyo, vita vingine vya maneno utavishinda kwa kuwa na nidhamu binafsi ya kusema baadhi tu ya mambo yanayokuhusu.

Ukweli ni kwamba, si kila mtu utakayemweleza mambo yako atayafurahia. Hutokea kwamba, wengine ukiwaeleza leo, kwa chuki zao binafsi, hawatasubiri hadi ifike kesho. Watatafuta kila njia kukuharibia kabisa maisha yako haraka iwezekanavyo. Inakupasa uchunge sana ulimi wako, binadamu wengine siyo wema hata kidogo.

Ni dhahiri kuwa kuna mambo mengine itakupasa uwaeleze watu unaowaamini kwa kupata ushauri. Pamoja na hayo, itakupasa upime uzito wa jambo lenyewe kabla ya kulisema. Si kila jambo ulilonalo moyoni linaweza kuelezwa kwa kila mtu. Yakupasa kuchagua ni jambo gani umweleze nani ili kukwepa matangazo.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Usitengeneze Mipaka Katika Kupenda

Alfreda George - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Neno linaloitwa kupenda kwa kawaida siyo geni sana kwa watu wengi ila utekelezaji wake ni mgumu sana. Mara nyingi watu huwa wanatekeleza neno upendo kimatabaka. Huwa wanaangalia uwezo wa mtu ndipo waweze kumpenda na upendo huo unakuwa na sababu. Wenye kulingana kiuchumi ndio wanakuwa katika tabaka moja. Sio rahisi kwa mtu usiye na uwezo kuwa na kundi moja na mwenye uwezo kwa sababu utakuwa huna lolote la kusema mbele yao. Ukiwa kwenye kundi hili la ‘’wazito’, tegemea dharau kutoka kwa wenye nacho. 

Katika hali ya kawaida, hakuna mtu asiye kuwa na jambo ambalo mwingine hana ama halijui. Sawasawa na vidole vya mikononi, pamoja na tofauti iliyopo, vingine ni vifupi, vingine ni virefu, ukweli ni kwamba vyote ni vya muhimu sana katika matumizi yake. 

Maandiko matakatifu yanatuagiza kuwa tupendane, na hii ndio amri kuu tuliyopewa. Pamoja na agizo hilo, bado huwa tunaweka mipaka kwenye amri hiyo. Hatutakiwi kuweka mipaka kwenye amri hiyo. Hatutakiwi kubaguana kwa sababu ya hali ya mtu, tupendane bila kujali tofauti zetu. Yatupasa tujue na tuzingatie kuwa binadamu wote ni sawa na kwamba sote tumeumbwa kwa makusudi maalumu na Muumba wetu ni mmoja. Upendo unatakiwa utawale katika maisha yetu.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Eti Mtoto Wa Kike Ni Nyanya, Ikikaa Sana Itaoza

Grace Mshanga - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Grace Mshanga (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Usemi huu unapingwa sana na watu wote wenye busara na akili timamu. Kwanza siyo sahihi hata kidogo kulinganisha binadamu na nyanya mbovu ama kitu chochote kile. Tunapoangalia suala la malezi ya mtoto wa kike tunaona kuwa anahitaji uangalizi wa hali ya juu zaidi kuliko mtoto wa kiume. Hii ni kutokana na maumbile yake, pia na nafasi ya mwanamke katika jamii, nafasi ya kuonewa. Kutokana na ukweli huo, tunaamini kuwa inampasa mtoto wa kike afundishwe katika kila hatua anayopitia ili ajue jinsi ya kujilinda na yote yatakayofuata katika kila hatua ya makuzi yake.

Usemi wa “Mtoto wa kike nyanya mbovu ikikaa sana itaoza”, umekuwa ukitumika sana hasa kwa baadhi ya jamii ya wafugaji na wale ambao bado wanaendeleza mila potofu. Ulinganisho wa nyanya mbovu na mtoto wa kike siyo sahihi hata kidogo. Wanaotumia usemi huu ni wale wanaoamini kuwa mtoto wa kike asipoolewa katika umri mdogo anakosa thamani. Fikra hii ni kinyume na ukweli kwani akiolewa mapema kuna madhara yanayoweza kumpata wakati wa uja uzito na hata kujifungua kwake kunakuwa ni hatari kubwa. Baadhi ya jamii hizo na wenye mila potofu huona kuwa hakuna haja ya kuwapa watoto wao wa kike haki ya elimu. Wakati mwingine huwasomesha hadi kumaliza elimu ya shule ya msingi tu.

Mara nyingine nyingine wazazi hata hudiriki kuwashawishi watoto wafanye vibaya mitihani yao ya kumaliza elimu ya shule ya msingi ili wakaolewe. Mtoto wa kike kusoma hadi Chuo Kikuu huonekana kuwa ni wazo baya kwani litawapotezea muda, umri utakuwa umekwenda sana. Kisingizio kikubwa eti ni binti akiwa na umri mkubwa mara nyingi huwa ni shida kupata mchumba, hii si kweli.

Fikra hizi ni potofu na pia ni za uonevu kabisa kwa sababu kwa kawaida, kijana anapomaliza chuo kikuu anaweza kuwa na umri wa miaka 22 hadi 27 ambao bado unakuwa ni umri muafaka wa kuolewa. Lakini pia ikumbukwe kuwa maendeleo hayaletwi na vijana wa kiume pekee yao. Uzoefu unaonyesha kuwa siku hizi, vijana wa kike kwa dunia ya leo wanaleta maendeleo makubwa zaidi kuliko vijana wa kiume. Ule usemi unaosema kuwa, “Ukimsomesha mwanamke unasomesha jamii nzima” unasisitiza ukweli huu.

Yatupasa tuwape haki ya elimu watoto wetu wote bila kujali jinsia zao. Watoto wote, awe mvulana ama msichana, ndio tegemeo la maendeleo kwa taifa letu. Hebu tuache ubaguzi usiokuwa na maana kwa maendeleo yetu.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Arts #Culture #Tanzania

Misukosuko Huleta Mafanikio

Alfreda George - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Maisha ya binadamu hayana formula maalum. Mara nyingi kwenye maisha, kufanikiwa kwa mtu hutegemea sana na uwepo wa jambo ambalo litamsukuma ili aweze kubadili taratibu za maisha yake. Kwa mfano, kuna watu ambao wanaona kuishi na mtu bila kulipa chochote ndio chanzo chao cha kufikia malengo yao. Ukweli ni kwanba watu wenye mawazo ya namna hiyo huishia kushindwa vibaya. Watu wa roho tegemezi hawawezi kuona kuwa wanatakiwa kufanya mambo yao wenyewe ili waweze kujitegemea.

Vijana wengi wa siku hizi ndivyo walivyo. Hupenda sana maisha ya dezo, maisha ya bure bure. Hawataki maisha ya kuanzia chini. Hupenda kuwa na mambo makubwa ambayo yako nje ya uwezo wao, mambo ya mkato. Tatizo kubwa ni kwamba hawajui kuwa hao wanaoonekana sasa hivi kuwa wanajiweza, wametoka mbali na walipitia vikwazo vingi sana hadi kufikia hapo walipo. Pengine itafika wakati ambapo inabidi umwambie tegemezi wako kuwa imetosha, aondoke ili akajifunze kujitegemea. Mara nyingi ujumbe kama huu huwa haupokelewi vizuri. Hapo ndipo huwa mwanzo wa kutokuelewana na ndugu. Visa na maneno kutoka kwa jamii huanza, huyu anasema hili, na yule anasema lile, ili mradi tu hali inakuwa ya kukoseshana amani. Wao wanachoona ni kuwa umemtendea vibaya ndugu yako kwa sababu umemfukuza. Kwa kawaida, huwa hawana muda wa kuangalia kwa undani wala kutafuta ama kuulizia sababu zilizopelekea ufanye hivyo, hata ufikie hatua ya kumfukuza ndugu yako. Kila mtu sasa ataziongelea habari zako ambazo sasa zitakuzwa kupindukia, kila mtu atasimuliwa. Wanaosikia habari hiyo watakuchukia sana na kukuona wewe ni mnyanyasaji. Sasa watu wataacha hata kutembeleana, urafiki, undugu utakwisha kwa sababu ambazo si za msingi.

Kutokana na akili ndogo ama kutojua, jamaa aliyefukuzwa na ndugu yake anashindwa kuelewa kuwa yale yaliyotokea ndio mtikisiko wake wa kumsogeza mbele kimaisha. Mtikiso huo alioupata utamfanya aamke na aanze kupambana na maisha kwa maendeleo yake ya bila utegemezi.

Yatupasa tukumbuke kuwa mambo mazuri yanakuja baada ya kutikiswa. Kuchukua ushauri ama kufuata maelekezo ni njia nzuri ya kujikwamua kimaisha. Tusione aibu kuchukua ushauri ama kufanya maamuzi magumu. Majaribu ni mtaji wa mafanikio. Ukijaribiwa usiogope kwani ni sehemu ya maisha na hivyo hayana budi kutokea. Bila mapito magumu, mara nyingi, mafanikio huwa ni ndoto.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Jitihada Haiondoshi Kudra

Tap Elderly Women's Wisdom for Youth (TEWWY)

Simulizi

by Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY).

Binadamu wanaamini kwamba mtu anapozaliwa tu, mambo yake yote katika maisha huwa yameshapangwa na Mwenyezi Mungu. Mathalani, riziki yake yote huwa imeshawekwa tayari, siku yake ya kufa na hata saa yake pia inakuwa imepangwa. Tunaamini kuwa hata mtu angetaka kubadilisha, uwezo huo inaonekana haupo kabisa. Mambo hayo au mipango hiyo inabaki kuwa kama vile alivyopanga Muumba wetu.

Mara nyingi, usemi huu unatumiwa kuwaliwaza watu ambao wamejitahidi au wamejaribu sana kufanya mambo fulani lakini hawakufanikiwa. Pengine hii inamaanisha kuwa ingawa mtu anaweza kuwa amejaribu sana kufanya jambo, hawezi kuyabadilisha yale yaliyopangwa na Mungu, yaani kudra ya Mungu. Hii inamaanisha kuwa asihuzunike sana kwani mambo hayo hayako ndani ya uwezo wake. Kwa upande moja, ni faraja nzuri kumpatia mhusika, lakini kwa upande mwingine, faraja hiyo inaweza ikamfanya mtu akajibweteka na kuwa mvivu kwa kisingizio hicho cha kuwa hiyo ndio kudra ya Mungu na hivyo hawezi kufanya chochote. Pamoja na kudra ya Mungu inabidi watu kufanya kazi kwa bidii kwani bidii katika kazi hulipa pia.

Usemi huu vile vile hutumiwa kumpa moyo mtu anayekabiliwa na shida asiyoweza kuiepuka, kwamba amuachie Mwenyezi Mungu, asipapatike wala asibabaike. Yote hii ni kuonyesha kuwa lile lililoandikwa au lililopangwa na Mungu, ndilo litakalokuwa tu na si vinginevyo.

Pia usemi huu unalinganishwa vizuri na ule usemao, “Liandikwalo, Halifutiki” ama ule wa “Riziki Hufuata Kinywa”. Misemo yote hii ni ile inayohusiana na kudra ambazo mara nyingi huchukuliwa kuwa hakuna chochote kinachoweza kubadilisha hicho kilichopo, kilichopangwa na Mungu.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Arts #Culture #Tanzania

Mtizamo Chanya Ni Muhimu Katika Maisha

Victoria Nakajumo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Victoria Nakajumo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Kati ya vitu vinavyotupotezea muda watu wengi, ni ile hali ya kutaka kujua watu gani wanatusema vibaya. Yaani unatumia muda wako mwingi kutafuta habari mbaya zinazosemwa kuhusu wewe kuliko muda unaoutumia kufanya mambo yako ili kutimiza malengo yako.

Unakuta muda wako wote unajihisi kuwa unasemwa vibaya, ukiona watu wawili wamekaa wanaongea unahisi wanakujadili wewe na kukusema vibaya, ukiona mtu wako wa karibu anaongea na simu unajificha kusikiliza ukihisi unaongelewa wewe.

Ndugu au mwenzi wako akiweka simu unaichukua na kuanza kuikagua kama kuna namna unasemwa kwa watu vibaya. Maisha ya namna hiyo siyo mazuri, ni mabaya, na si hivyo tu, yatakukosesha furaha na amani na hatimaye utashindwa kujiamini. Amua kuishi maisha ya furaha, maisha ya kujiamini, kwa sababu haijalishi wewe unaona umekamilika kiasi gani ama ni bora kuliko watu wengine kwa kiasi gani. Binadamu ameumbwa kusemwa na watu, anaweza kusemwa kwa mazuri ama kwa mabaya, yote yanawezekana. Siyo rahisi hata kidogo kuwazuia watu kukusema. Ni kawaida kusemwa na wala usitishike. Hatuna mamlaka ya kupanga nini kisemwe dhidi yetu. Chochote kinaweza kusemwa juu yako. Cha msingi, kama wewe ni mtu mzuri/mwema maneno ya watu, yawe mabaya ama mazuri hayatakufanya wewe kuwa mbaya. Hali kadhalika, maneno yoyote mazuri, yatakayosemwa juu yako hayatakufanya wewe kuwa mzuri. Kama wewe ni mbaya, utabaki kuwa mbaya tu. Cha msingi, yatupasa tujitahidi kuishi maisha yanayokubalika mbele za watu na mbele za Mungu. Mengine yawayo yote, huwezi kuyazuia.

Watu watabaki kuwa watu, na si vinginevyo. Wekeza muda wako kuyatenda yaliyo mema, timiza kusudi lako la hapa duniani. Tukumbuke kuwa muda tuliopewa kuishi hapa duniani ni mfupi sana, una kikomo. Hatukuja kuishi milele hapa duniani. Ukianza kuhangaika kila siku kutafuta mbaya wako ni nani, na nani wanakusema vibaya, hutafika kule unakotaka kufika. Utashindwa kutimiza malengo yako. 

Kuanzia leo jitahidi kubadili mtazamo wako juu ya vitu na watu. Jitahidi kuwa na mtazamo chanya. Maisha ndivyo yalivyo. 

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Jogoo Awike Asiwike, Kutakucha Tu

Avelina Hokororo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Avelina Hokororo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Mara nyingi tunasikia watu wakisema msemo huo hapo juu. Msemo huu una maana kubwa sana kwa maisha yetu ya hapa duniani. Binadamu tuko tofauti, kuna wengine kazi yao kubwa wanayoiweza ni kuhakikisha kuwa wanakwamisha juhudi za wengine ili mradi tu wasifanikiwe. Hufanya hivyo wakiwa na furaha mioyoni mwao kuwa watazuia maendeleo ama mafanikio ya wenzao.

Ukweli ni kwamba siyo lazima malengo yao ya kukukwamisha yafanikiwe. Pamoja na kushindwa kwao bado wataendelea kujaribu kila njia ili azma yao ifanikiwe. Watu wa aina hii huwa hawachoki. Wanaweza wakafanya hivyo kwa muda mrefu lakini kutokana na juhudi zake za kufanya kazi mtu huyu, bila kukata tamaa pamoja na kumtegemea Mungu, mwisho wa siku hufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana.

Hatimaye, baada ya kuona kuwa jitihada za kumwangusha zimeshindikana, wale watesi wake hubaki wakishangaa. Hawajui kuwa mafanikio ya mtu mwenye haki hayazuiliki bali yanaweza kuchelewesha tu na si vinginevyo. Cha msingi, yatupasa tujifunze kuwa wavumilivu katika maisha yetu, magumu tupitiayo yasitukatishe tamaa bali yatuimarishe zaidi katika utendaji wetu wa kazi. Matatizo ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Matatizo hutufundisha, hutujenga na kutufanya tuwe bora kadri siku zinavyoenda. Na ndio maana ni sahihi kabisa kusema kuwa hata jogoo asipowika, ni lazima kutakucha tu, hakuweza kuendelea kuwa usiku, mwanga utakuja na siku mpya itaanza vyovyote na iwavyo.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #ArtTherapy

Kifo Cha Wengi Ni Harusi

Tap Elderly Women's Wisdom for Youth (TEWWY)

Simulizi

by Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY).

Kwa kawaida, msiba ukiwapata watu wengi, kwa kiasi fulani hauhuzunishi sana kama ukimpata mtu mmoja peke yake. Hii ina maana kuwa msiba wa watu wengi ni mzigo unaobebwa kwa kushirikiana na watu wengi. Unaweza kusema kuwa uzito wake hauelemei sana kutokana na wengi kuguswa na jambo hilo.

Msiba wa mtu mmoja unaelemea sana kwa sababu mtu ana ubeba yeye peke yake, anakuwa hana msaidizi au mtu wa kumpunguzia ama kumgawia machungu aliyo nayo.

Usemi huu hutumiwa kuwatia watu moyo ili waweze kufanya, mathalani, mambo ya hatari na uonevu kwa ushirikiano ili waweze kupata ufumbuzi wa pamoja. Inawezekana kwenye jamii fulani kunakuwa na kundi la watu ambalo linaamua kuwanyanyasa wananchi kwa kuwanyang’anya, mfano, ardhi kwa visingizio visivyo vya msingi zaidi ya uonevu tu. Wananchi hawa wakipaza sauti kwa pamoja wanaweza wakalishinda kundi hilo la uonevu na unyanyasaji kwa urahisi zaidi kuliko angekuwa ni mtu mmoja anayeonewa na kundi hilo.

Hapa pia, usemi wa “Umoja ni Nguvu, Utengano ni Udhaifu” unaweza ukatumika barabara na ukaleta maana hiyo ya msiba wa wengi ni sawa na harusi.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Arts #Culture #Tanzania

Ajaye Kisimani Mbele, Hunywa Maji Maenge

Tap Elderly Women's Wisdom for Youth (TEWWY)

Simulizi

by Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY).

Msemo huu unatumika na makabila mengi sana hapa nchini. Popote pale msemo huu utakapotumika, maana yake ni moja tu. Neno ‘mbele’ lina maana kabla ya wengine. ‘Maji maenge’ ni yale maji safi yaliyotuama vizuri na takataka zake zinakuwa zimetulia chini.

Kwa hiyo maana ya usemi huu ni kwamba mtu yeyote atakayekwenda kisimani kabla ya watu wengine, au mahali popote palipo na maji, kama vile bwanani, kwenye madimbwi ama mtoni, atayakuta maji yametulia tuli na takataka zote ziko chini. Maji yanakuwa katika hali ya usafi kwa sababu yanakuwa hayajakorogwa ama kutikiswa na wachotaji wengine.

Usemi huu unatufundisha yafuatayo:

  1. Umuhimu wa kufanya mambo mazuri mara tunapoweza bila kungoja ngoja. Kama ule usemi usemao: ‘Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako’. Kadri unavyochelewa kutenda jambo ndivyo utakavyoambulia mambo yasiyokuwa mazuri ama yasiyo na tija.
  2. Kwa matokeo mazuri, yatupasa tujitahidi kuwa wa kwanza kufanya jambo. Ni dhahiri kuwa yule atanguliaye kufanya jambo, ndiye huwa anafaidi zaidi. Tusikubali kuwa wa mwisho katika kufanya mambo na hasa pale inapobidi ili tuweze kufaidi mambo mzuri ambayo yanakuwa bado hayajaharibiwa na waliotutangulia.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Arts #Culture #Tanzania

Ajengaye Siye Alalaye

Tap Elderly Women's Wisdom for Youth (TEWWY)

Simulizi

by Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY).

Kwa kawaida, mtu anapojenga nyumba yake anakuwa na mategemeo makubwa. Tegemeo lake la kwanza ni kuwa atakaa humo, yaani ataishi ndani ya nyumba hiyo.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa hiyo siyo lazima iwe hivyo. Mtu anaweza akajenga nyumba yake lakini akafa, pengine baada ya kukaa humo kwa siku chache tu. Nyumba yake hiyo inaweza kurithiwa na watoto ama ndugu wengine wa karibu. Warithi hao wanaweza wakaishi ndani ya nyumba hiyo kwa muda mrefu sana kiasi kwamba inakuwa vigumu kwa watu wengine kumjua mhusika mkuu alikuwa ni nani, yaani aliyeigharamia hiyo nyumba mpaka ikasimama na kuwa nyumba.

Usemi huu unatufunza kuwa tunapofanya jambo zuri tusitazamie kuwa ni lazima tufaidike nalo kwa kuwa tumelifanya sisi. Tunatakiwa tusiwe na choyo kwa kutaka wengine wasinufaike nalo. Tunapofanya jambo jema tulifanye kwa kuwa ni wajibu wetu, mathalani, kujenga nyumba, ni wajibu wa kila binadamu yeyote kufanya hivyo. Kujenga nyumba ni jambo jema, jambo la busara.

Endapo jambo tunalolifanya litakuwa na manufaa kwetu, itakuwa sawa kwani kunufaika na jasho letu ni jambo la heri, ni jambo jema. Na ikiwa hatutanufaika nalo, bali ni watu wengine ndio watanufaika, yatupasa tusisononeke wala kuona kuwa ni vibaya. Ndio maana ya msemo huu kuwa anayejenga nyumba si lazima aje alale humo. Thawabu utakazopata ni nyingi kutokana na jasho lako kuwanufaisha watu wengine.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Arts #Culture #Tanzania

%d bloggers like this: