MTAKA YOTE KWA PUPA HUKOSA YOTE

Sakina Bushiri
Wisdom&Wellness Counselor

Mangaya, Dar-es-Salaam

Usemi huu hutumika kuwakanya watu wasiokuwa na misimamo thabiti, wenye tamaa, ambao wanapenda kushiriki katika kila jambo litokealo kwa wakati moja. Wasipokuwa waangalifu, tabia hii inaweza ikawafanya washindwe kufanikiwa hata jambo/shughuli moja. 

NDEGE MOJA MKONONI NI WA THAMANI KULIKO KUMI WALIO PORINI

Rustica Tembele
Founder & CEO

Maana yake ni kidogo chochote ulicho nacho ni cha thamani kuliko vingi ambavyo haviko mikononi mwako. 

Msemo huu unaweza kutumika kwa kuwaasa watu wenye tabia ya kudharau kidogo walichonacho na kushabikia/kutamani kikubwa wasichokuwa nacho.. 

MTAKA NYINGI NASAHA, HUMKUTA MINGI MISIBA

Sakina Bushiri
Wisdom&Wellness Counselor

Mangaya, Dar-es-Salaam

Hii hutumika kuwaasa wale wanaopenda kufanya urafiki na kila mtu au kuwafanya kama ndugu zao hukutwa na misiba mingi kwani kila tatizo la mmoja wao litamhusu yeye pia.

Msemo huu unaweza kutumika kwa watu ambao wanapenda kujionyesha ni maarufu na hivyo kutaka waonekane wanashiriki kila jambo litokealo, ukweli ni kwamba siyo rahisi kuwepo kila mahali.

NDEGE MJANJA HUNASA KWENYE TUNDU BOVU

Rustica Tembele
Founder & CEO

Inaweza kuwa na maana ya mtu kufikishwa pabaya pale anapofanya uchaguzi uliopitiliza wa kitu chochote na hatimaye kupata kitu kisicho kizuri. Mathalani, mwanaume anayechagua sana mke au mwanamke anayechagua sana mume anaweza kuishia kupata mke/mume asiyefaa.

Usemi huu unaweza kutumika kwa kuwaasa watu wanaofanya chaguzi zilizopita kiasi kwenye maisha.

HABA NA HABA HUJAZA KIBABA

Sakina Bushiri
Wisdom&Wellness Counselor

Pugu, Dar-es-Salaam

Hii hutumika kuwahimiza watu kuweka akiba, kwani kwa kuweka kidogo kodogo hatimaye utakuwa na akiba ya kutosha 

Msemo huu hutumika kuwaasa watu ambao wana tabia ya kutumia kila wapatacho bila kuweka akiba angalau kidogo. Watu wa namna hii hupata matatizo huko mbeleni kwa kukosa hata mahitaji ya msingi.

NIAMBIE RAFIKI ZAKO NI NANI, NAMI NITAKUAMBIA WEWE NI NANI

Rustica Tembele
Founder & CEO

Maana yake, watu wakijua marafiki unaofuatana nao wanaweza wakajua wewe ni mtu wa aina gani kutokana na tabia za wale rafiki zako, mathalani, kama wana tabia mbaya basi na wewe hautakuwa tofauti nao, vile vile wakiwa na tabia nzuri basi na wewe utafanana nao.

Msemo huu unaweza kutumika pale mtu anapokuwa na tabia zisizotabirika, anapenda kuigaiga na kufanya vitu visivyo vya kawaida. Kwa vile unashindwa kumjua vizuri basi unaweza kumwambia akuambie marafiki zake ni nani ili ujue ni kundi gani unaweza kumuweka.