UMOJA NI NGUVU, UTENGANO NI UDHAIFU

Caroline Swai
Wisdom&Wellness supervisor

Kigamboni,Kinondoni & Ubungo, Dar-es-Salaam

Tunaposhirikiana kufanya shughuli zetu pamoja, inakuwa rahisi kumaliza haraka kuliko ya kipekee na kujitenga – hali ambayo inachukua muda mrefu na kupunguza ufanisi.

CHAKULA KIIVAPO WATOTO HUWA WANAKIZUNGUKA HARAKA, LAKINI WAKATI WA KAZI HUTOA SABABU NYINGI

Grace Mshanga
Wisdom&Wellness supervisor

Temeke & Ubungo, Dar-es-Salaam

Watoto wana kawaida kuwa chakula kinapokuwa tayari huzunguka haraka na kuanza kula lakini wakipewa kazi hufanya kwa kinyonge. Hit ni kuwafundisha watoto kuwa wakiwa katika umri mdogo waanze kujifunza kufanya kazi ndogondogo mfano, kuosha vyombo na kufagia sio kungoja chakula tu.

BAADA YA JUA KUZAMA, WASICHANA HAWARUHUSIWI KUTOKA NYUMBANI KWAO

Grace Mshanga
Wisdom&Wellness Supervisor

Temeke & Ubungo, Dar-es-Salaam

Jua likizama na kiza kikianza kuingia wakati huwezi kumtambua vizuri anayekuja mbele yako, wasichana hawaruhusiwi kutoka nje ya nyumba yao. Hii inawalinda wasichana ili  wasitendewe mabaya au kuonewa na wavulana maana wakati huu wavulana huwa matembezini. Pia hii ni njia mojawapo ya kuwafundisha watoto wa kike kuwa na tabia njema.

USIPOZIBA UFA UTAJENGA UKUTA

Sakina Bushiri
Wisdom&Wellness Counselor

Mangaya, Dar-es-Salaam

Usemi huu hutumika kuhimiza au kuwafunza watu kurekebisha mambo kabla hayajaharibika kabisa. Kwa mfano, nguo ikitatuka kidogo shona usiiache ichanike yote utakuja kushindwa kuirekebisha. Kwa hapa ilivyotumika ukuta ukiwa na ufa uzibe la sivyo utaanguka na kukubidi ujenge ukuta mzima.