Kidole Kimoja Hakivunji Chawa

Avelina Hokororo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Avelina Hokororo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Kuna kisa kimoja ambacho ni cha kweli kabisa na kimetokea hivi karibuni. Kisa hiki kinaelezea jinsi bwana mmoja alivyokuwa mbinafsi. Bwana huyu alipenda kufanya mambo yake kwa siri, peke yake. Ubinafsi au usiri huu ulikuwa mpaka kwa mke wake, kwani alikuwa hamshirikishi kwa jambo lolote la maendeleo, liwe dogo ama kubwa. Mathalani, hata kama akitaka kujenga, ama kusafiri, atamwambia mke wake siku anaondoka. Alikuwa akiamini kuwa wanawake wengine huwa wana nuksi au mikosi na hivyo ukiwaambia mipango yako inaweza isifanikiwe. 

Siku moja katika pitapita zake, aliona gari jipya lipo gereji fulani na kwamba lilikuwa linawekwa sawa ili liweze kuingia barabarani. Kwa vile alikuwa na hitaji la gari kwa muda mrefu, alimuuliza kijana mmoja aliyekuwepo pale gereji, “Je gari hilo linauzwa?” Yule kijana alimjibu, “Ndiyo bosi, linauzwa”. Bila kuchukua muda na kufikiri, alipatana na huyo kijana aliyekuwa amemuuliza. Kijana huyo alijitambulisha kuwa yeye ndiye mwenye gereji na hivyo bila kusita, alimwambia bei ya hiyo gari. Huyo bwana kutokana na uhitaji wake, bila kuchelewa, alilipia kwa bei aliyoambiwa. Aliambiwa aende baada ya siku tatu na kwamba atalikuta gari likiwa tayari kwa kulichukua.

Maskini, kumbe aliyepatana naye hakuwa mwenye gareji wala nini, bali alikuwa mfanyakazi tu, tena kibarua na ndiye aliyemlipa pesa nyingi. Bwana huyu hata risiti alikuwa hakupewa. Walipatana kuwa siku atakapokuja kuichukua gari ndipo atakapopata risiti na kila kinachohusiana na manunuzi ya gari hilo. 

Siku ya kuchukua gari ikafika. Akaenda pale gereji. Kwa mshangao mkubwa, alikutana na baba mkwe wake anakabidhiwa gari alilokuwa amelilipia yeye. Hakuamini macho yake. Hata hivyo jamaa alijikaza na kumuulizia yule kijana aliyekuwa amefanya naye mazungumzo ya gari na kufanya malipo. Aliendelea kushangaa zaidi pale alipoambiwa kuwa yule kijana ni kibarua tu ambaye huja kufanya kazi pale kama kuna kazi inakuwa imejitokeza. Waliendelea kumwambia kuwa kwa leo alikuwa hajafika, kwani hakuna kibarua chochote cha yeye kuja pale.

Baba mkwe naye aliingilia kati na kumuuliza. Maskini yule bwana hakujibu chochote. Badala yake, yule bwana alirudi nyumbani kwake akiwa na majonzi yasiyo kifani. Majonzi hayo yalimpelekea kupata msongo mkali wa mawazo. Hivi sasa amebaki anaongea peke yake. Kulia anataka, kucheka anataka, ili mradi tu hajielewi, amechanganyikiwa. Waswahili wameanza kumpa majina ya kumnyanyapaa ya ‘dish limeyumba’ nk. Amebaki kujiapiza tu kuwa siku akimuona yule kijana atamchinja kwa mikono yake mwenyewe.

 Alipofika nyumbani, mkewe kuona hali ya unyonge wa mume wake, alimuuliza yaliyomkuta. Hakusita kumweleza mkasa mzima uliompata bila kutegemea. Mkewe bila kumficha, aliongeza chumvi kwenye kidonda chake. Alimwambia kuwa yeye alikuwa anajua kuwa baba yake alikuwa amenunua gari. Alimweleza pia kuwa hata gereji aliyopeleka gari hiyo baada ya kutoka bandarini alikuwa anaijua. Aliposikia hayo, mumewe alijibaraguza na kusema kuwa, eti alitaka kum-‘surprise’. Lakini, hiyo haikuwa ni kweli, bali ulikuwa uongo mtupu. 

Yule bwana hakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kumuomba msamaha mke wake kwa kushindwa kumuamini. Aliapa kwa miungu yote aijuayo kuwa kuanzia sasa atakuwa akimueleza mke wake kila mpango alio nao ili kukwepa yale yaliyompata yasijirudie tena.

Kisa hiki kinatufundisha umuhimu wa kushirikisha mipango yetu, hasa kwa wake au waume zetu. Kufanya vitu chini chini vinaweza vikatugharimu sana kama ilivyokuwa kwa huyu jamaa. Kuna mipango mingi sana ambayo imewaingiza watu mahali pabaya kwa kukosa kuwaamini wenza wao. Tuepuke kupata matatizo ya afya ya akili ambayo tunaweza kuyakwepa kwa kuwashirikisha watu wa karibu sana nasi, hususani, wenza wetu. Usemi wa kidole kimoja hakivunji chawa, unakazia simulizi ama kisa hiki.

The Healing Hands Project

The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: