Unachokikataa Leo, Kinaweza Kukufaa Kesho

Alfreda George - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Kwa kawaida, binadamu tuna tabia ya kuangalia ya leo na siyo ya kesho yetu. Kuna kijana mmoja alimpa mimba binti fulani. Kwa kuogopa, huyo binti hakuweza kumueleza kijana mapema kuhusu mimba yake. Alikuja kumweleza baada ya miezi mitano kupita. 

Kijana kusikia habari hizo, aliruka futi kumi na tisa juu. Alikataa kata kata, na kwa hasira, alimwambia binti huyo maskini kuwa hakuwa tayari kuitwa baba wa mtoto atakayemzaa. Bila aibu, alimwambia huyo binti kuwa ana na mtu wake ambaye amepanga kuoana naye. Alimpa kibali cha kuitoa hiyo mimba kama anataka. 

Binti alikuwa ni mcha Mungu sana, alikataa kutoa mimba. Badala yake, kijana alimwambia binti kuwa, kama hataki kufanya anayomuelekeza, basi asimjue na kwamba hana mpango naye wa aina yoyote ile. Bahati mbaya mama yake yule binti alikuwa amefariki, na hivyo alikuwa analelewa na mama wa kambo. Hali ya ujauzito haikukubalika na mama wa kambo na hivyo alifukuzwa pale nyumbani. Ikawa tabu kweli kweli kwa binti yule.

Baada ya kufukuzwa nyumbani, binti alianza kuishi maisha magumu sana. Aliishi kwa kufanya vibarua kwa watu mpaka alipojifungua. Wasamaria wema ndio walikuwa msaada mkubwa kwake. Alimlea mtoto wake katika mazingira magumu sana. Mungu ni mwema, mtoto alikua, akasoma vizuri na akabahatika kupata kazi nzuri. 

Kwa bahati mbaya, yule kijana aliyeikataa mimba ya binti yule, hakubahatika kupata mtoto kwenye ndoa yake aliyokuwa akiiringia. Jitihada za kupata mtoto ziligonga  mwamba. Katika pitepite zake za hapa na pale, alifanikiwa kupata habari ambazo zilikuwa na ukweli ndani yake. Waswahili husema, “watu hawakunyimi neno”. Kuna jamaa ambaye alikuwa anamfahamu yule kijana msomi aliyekuwa amekataliwa akiwa mimba kwa mama yake. Jamaa huyu alimweleza yule baba yake kuhusu habari zake na mafanikio ya mtoto huyo.

Siku moja baba yule alifika ofisini kwa ‘mtoto’, akajitambulisha kwa yule ‘mtoto’ ambaye alimshangaa kwa maana alikuwa hajawahi kumuona hata siku moja. Kwa upole, mtoto alimwambia huyo baba, aondoke ili aende kwanza akazungumze na mama yake. Baba alichoka sana na alijuta sana.

Mtoto alikuwa jasiri, na wala hakuwa na kinyongo. Alizungumza na mama yake ambaye bila kumficha alimwambia ukweli kuwa, “ni sawa, mwanangu, huyo ni baba yako japo alinikataa nilipokuwa mjamzito na kwamba asingekuwa na habari nami na mtoto nitakayemzaa”. Aliendelea kumwambia mtoto wake kuwa, “lakini kama unaweza kumsaidia fanya hivyo, usiangalie yaliyopita”. Kama waswahili wasemavyo, ‘Yaliyopita si ndwele, tugange ya hayo”, wawili hawa, yaani mama na mtoto, waliganga yajayo.

Hii ni hadithi ya kweli, na tuna mengi ya kujifunza. Baadhi ya yale tunayoweza kuchota kwenye simulizi hii ni haya yafuatayo:

1. Tusiwe wepesi kukataa mimba/watoto kwa kuogopa majukumu yaliyo mbele yetu. Kama ulikuwa na mahusiano ya kimapenzi na binti, yakupasa ukubali kubeba mzigo unaopewa na halafu kama wasiwasi bado unakuwepo, ni vema mfanye mpango wa kufanya asidi nasaba (DNA) ili kujua uhalisia na ukweli kuhusu nasaba za mtoto huyo, kama wewe kijana ni baba wa mtoto huyo ama laa. 

2. Hakuna mtoto anayeomba kuzaliwa na baba huyu wala mama yule. Tukwepe kuwatesa watoto wasio na makosa.

3. Kulazimisha binti atoe mimba ili kukwepa majukumu ni dhambi, labda kuwe na sababu za kiafya za kitaalamu za kufanya hivyo. 

4. Binti usikubali kutoa mimba, hebu tafakari kwa kina, endapo mama yako angetoa mimba yako wewe leo hii ungekuwepo?

5. Wazazi/walezi, tuwe makini katika malezi ya watoto wetu ili wasifikie mahali ambapo wanatupa watoto kwa sababu ya kuogopa kulea. Wakati mwingine, sisi wazazi/walezi tunachangia kwa kiasi kikubwa vijana wetu kufikia maamuzi hayo ya kinyama, ya kutoa mimba. 

6. Tuwape nafasi watoto wazaliwe kwa sababu ni haki yao kuzaliwa, lakini pia hujui huyo kiumbe kesho huenda akawa wa msaada sana kwako. Mungu haleti kiumbe hapa duniani kimakosa, huletwa kwa makusudi maalum. Mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa mtu ni Mungu peke yake.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO’s mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: